Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul Islam wal-Muslimin Sheikh Ali Al-Khatib, Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia nchini Lebanon, katika hotuba yake alisisitiza misingi thabiti ya msimamo dhidi ya uchokozi wa Israel, ikiwa ni pamoja na kuondoka kikamilifu, kurejea kwa wakazi, kuanza ujenzi upya, kuachiwa huru wafungwa na kufanya mazungumzo kuhusu mkakati wa ulinzi.
Sheikh Al-Khatib alisema: Katika mazingira ambayo vita vimeongezeka, mashinikizo ya kimataifa yamezidi na uchokozi wa Marekani na Israel unaendelea kwa lengo la kulazimisha hali mpya za kisiasa na kiusalama kwa watu wa eneo hili kupitia nguvu, ugaidi na vitisho, tulitamani kusherehekea Idi hii katika miji yetu yote, vijiji vyetu, nyumba zetu na misikiti yetu; lakini majaliwa yamekuwa kwamba tupitie mtihani huu kutokana na uchokozi unaoendelea wa Israel unaowalenga watu pamoja na majengo.
Hii si mara ya kwanza kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kutujaribu kwa subira na uthabiti mbele ya dhulma na uchokozi, ninyi mmevumilia, mnaendelea kuvumilia na mnazitoa muhanga wa nafsi zenu na mali zenu za thamani katika njia ya kulinda heshima na utukufu ambao haukubali maisha ya udhalili na unyonge.
Aliongeza kuwa: Huu ndio Muqawama wenu ambao watu wake wameyatoa maisha yao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ili kuilinda heshima hii, na umekuwa ukimpiga adui mapigo yenye maumivu makali ambayo yamemfanya kuelekea kwenye vitisho na kuwatisha watu, licha ya kwamba mizani ya nguvu za kimada iko upande wake; jambo ambalo baadhi ya watu hututuhumu kwa sababu yake, hata hivyo; katika mizani yetu ya kiroho na ya Kimungu jambo hilo halina nafasi yoyote.
Imam Hussein (as) kule Karbala hakulitilia maanani jeshi kubwa la Bani Umayyah, na kauli yake mashuhuri ilikuwa: “Naapa kwa Mwenyezi Mungu, sitawapa kiaga cha udhalili wala sitakubali kujisalimisha kwenu kama mtumwa.”
Sisi tupo juu ya dini ya Bwana wa Mashahidi Imam Hussein (as) na babu yake Mtume Mtukufu (s.a.w.w), na hatuwezi kuwa wanyonge wala watumwa mbele ya ujeuri huu wa kinyama ambao unatekeleza aina mbaya zaidi za mauaji, uharibifu, mauaji ya halaiki na kuwafanya watu wakimbie makazi yao.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mashia alisema: Imekuwa wazi kwa kila mtu kuwa; vita vya uchokozi vya Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Lebanon vimeshindwa kufikia malengo yake, ambayo yalikuwa ni kuuangusha mfumo wa Iran na kuuangamiza Muqawama nchini Lebanon.
Kwa sasa serikali ya Marekani inazuia kufikiwa kwa makubaliano ili ionekane mbele ya wananchi wake na wapinzani wake wa kisiasa nchini Marekani kuwa imepata ushindi, wakati huo huo adui wa Kizayuni pia analeta tamaa za kupindukia kwa lengo hilo hilo, yaani kujenga taswira ya ushindi ili kukabiliana na wapinzani wa kisiasa wa Waziri Mkuu wake.
Aliendelea kusema: Lakini kwa mtazamo wetu, taswira halisi ya vita hivi inapita zaidi ya maana hizi za kimada na za muda mfupi na inatukumbusha vita vya kihistoria vya zamani ambavyo vilifuatana na utamaduni wa kikoloni na wa kiitikadi; jambo ambalo linaweza kuendelea kwa muda mrefu, japokuwa kuna juhudi zinazoendelea sasa za kuvisimamisha.
Katika muktadha huu, inaonekana kuwa; suala la Lebanon ni miongoni mwa mambo makuu yanayozuia kufikiwa kwa makubaliano yanayotarajiwa, kwa sababu adui wa Kizayuni anasisitiza kuendelea kulifungua suala hilo, wakati Jamhuri ya Kiislamu inaliona kuwa ni miongoni mwa vipengele muhimu vya makubaliano.
Jambo hili linatulazimisha kuishukuru Iran kwa msimamo huu wa kimsingi; msimamo ambao tulitamani serikali ya Lebanon pia ingeenda sambamba nao, badala ya kuingia katika mazungumzo bila kuwa na karata yoyote ya ushindi, ambayo tunaamini yataendelea katika mfumo wa kuchelewesha na kupoteza muda bila matokeo.
Sheikh Al-Khatib pia alisema: Kuongezeka kwa mashambulizi ya Israel tuliyoshuhudia katika siku zilizopita kunaonesha wazi hasira ya viongozi wa adui dhidi ya juhudi zozote za kusimamisha vita katika eneo hili. Sasa imekuwa wazi kwamba timu inayotawala katika utawala wa Kizayuni inataka vita hivi viendelee ili kujinasua kutoka katika mkwamo wake wa ndani sambamba na kukaribia kwa uchaguzi wa Israel.
Jambo la kushangaza ni kwamba; adui anataka usitishaji vita wa upande mmoja tu, yaani kutoka kwa Muqawama pekee, kama ilivyotokea katika miezi kumi na mitano iliyopita, na kwa mtazamo wetu jambo hilo halitatokea.
Aidha usitishaji vita lazima uwe wa pande zote au usiwepo kabisa, kwa sababu kuwaua sisi na kubomoa nyumba zetu hakupaswi kuruhusiwa huku kujibu mashambulizi ya jeshi la adui kukichukuliwa kuwa ni jambo la haramu.
Kwa vyovyote vile, tunasisitiza tena misingi yetu ambayo haikubali maridhiano wala kurudi nyuma:
Kwanza: Kuondoka kikamilifu na kwa jumla kutoka ardhi za Lebanon.
Pili: Wananchi kurejea katika miji yao, vijiji vyao na nyumba zao.
Tatu: Kujenga upya yale yaliyoharibiwa.
Nne: Kuachiwa huru wafungwa wote kutoka magereza ya Israel.
Tano: Kuitisha mazungumzo ya kitaifa kwa ajili ya kuweka mkakati wa ulinzi kwa msingi wa hotuba ya kiapo na taarifa ya wizara.
Mwisho, Sheikh Al-Khatib alisema: Enyi ndugu, katika siku hizi zenye baraka tunawaita nyote kujifunza kutokana na maadili ya Hija na Idi ya Adh-ha katika subira, unyenyekevu, kujitolea, ushirikiano na kujiepusha na mapambo ya dunia.
Pia katika tukio hili tunatoa wito wa kuongeza mshikamano, ushirikiano na kuwasaidia zaidi ndugu zetu waliolazimika kuhama makazi yao katika maeneo yote, kwa sababu mgogoro umechukua muda mrefu na mahitaji yake yameongezeka katika nyanja zote.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu airejeshe Idi hii kwa Walebanon, hususan Waislamu, ikiwa imeambatana na usalama, ushindi, utulivu, kheri na baraka.
Maoni yako